Sunday, February 24, 2013

SWANSEA YATWAA TAJI LA CAPITAL ONE CUP

Swansea imefanikiwa kutwaa taji lao la kwanza baada ya kuifunga timu kutoka daraja pili ya  Bradford katika fainali ya   Capital One Cup. Swansea ilikwenda mapumziko ikiwa magoli mawili huku mlinda mlango wa Bradford  Matt Duke kulimwa kadi nyekundu. Hadi mwisho wa mchezo Swansea iliibuka na ushindi wa goli 5
 
 

 

Wednesday, February 20, 2013

RAISI MWAI KIBAKI AWASILI NCHINI KUWAAGA WATANZANIA

Rais Mwai kibaki wa Kenya akikaribishwa  kwa maua na Mwanafunzi Tazmina Rasul(6) muda mfupi baada ya kuwasili nchini kwa ziara ya kiserikali (State Visit) ya siku mbili huku mwenyeji wake Rais Dkt.Jakaya Kikwete akiangalia.
Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete akimkaribisha Rais Mwai Kibaki wa Kenya muda mfupi baaada ya kuwasili katika uwanja wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ziara ya kiserikali (State Visit) ya siku mbili.
 

JAJI MKUU KENYA ADAI KUTISHWA KISIASA


Jaji mkuu wa Kenya Willy Mutunga,ametangaza kuwa anatishwa na baadhi ya wanasiasa na mkuu wa utumishi wa umma vitisho ambavyo anavitasfiri kama njama ya kumshinikizwa kutekeleza maslahi yao.

 

Madai haya yanajiri wakati Kenya ikijiandaa kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika chini ya wiki mbili.

 

Jaji Mutunga ameelezea kuwa alipokea vitisho hivi karibuni wakati kesi iliyowahusisha mgombea wa urais Uhuru Kenyatta na mgombea mwenza wake William Ruto ilipokuwa inasikilizwa.

 

Wawili hao ni washukiwa wa uhalifu wa kivita katika mahakama ya ICC na mahakama kuu ya Kenya wiki jana ilipaswa kuamua ikiwa washukiwa hao wanaweza kugombea urais au la.

 

Uamuzi uliotolewa na mahakama hiyo hata hivyo ulisema kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kuamua kesi hiyo na kwamba mahakama ya juu zaidi Kenya ndiyo ina uwezo pekee kutoa uamuzi.

 

Jaji mkuu Willy Mutunga alisema kuwa ujumbe wa barua aliyopkea ulikuwa unamtisha kuwa angetendewa jambo baya na kundi haramu la Mungiki.

 

Kundi hilo pia lilihusishwa na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 ambapo ilisemekana kuwa Uhuru Kenyatta alidaiwa kulitumia kushambulia watu wa kabila la Kalenjin mkoani Rift Valley.

 

Mutunga aliituhumu serikali kwa kumfanyia dhulma baada ya kuamrishwa na afisaa mmoja wa uhamiaji kusafiri kwenda Dar es Salaam kwani hakuwa na idhini ya mtumishi mkuu wa umaa Francis Kimemia.

 

Bwana Mutunga alisema hatishiki na kuwa hahitaji idhini kutoka kwa Kimemia kabla ya kusafiri kwenda nje ya nchi.

 

Pia ameelezea wasiwasi kuwa majaji wanatishwa kisiasa huku nchi ikiwa inaelekea katika uchaguzi mkuu.

 

Mutunga amesema hatatishika kwani amekuwa mmoja wa wapiganiajai wa demokrasia Kenya na kwamba yuko tayari kwa lolote wanalompangia.

 

Chini ya uongozi wa jaji mkuu huyu, idara ya mahakama imeweza kusifiwa kwa mageuzi makubwa kwani sasa inaonekana kuwa huru na kuwa ni vigumu kuwashawishi majaji kuegemea upande wowote

RAISI WA ZANZIBAR ATOA HESHIMA ZA MWISHO KWA MAREHEMU PADRI MUSHI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein,akiwasalimia wananchi wakati alipofika katika Kanisa la Minaramiwili Mjini Zanzibar kutoa salamu ya Mwisho kwa Padri Evarist Gabriel Mushi,aliyefariki kwa kupigwa risasi na watu wasijuilikanwa Jumapili iliyopita,na atazikwa leo Kijini Kitope Wilaya ya Kaskazini B Unguja.
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein,(kushoto) akitoa salamu ya Mwisho kwa mwili wa Marehemu Padri Evarest Mushi,katika Kanisa la Minaramiwili Mjini Zanzibar, Padri Gabriel Mushi,aliyefariki kwa kupigwa risasi na watu wasijuilikanwa Jumapili iliyopita,na atazikwa leo Kijini Kitope Wilaya ya Kaskazini B Unguja,(katikati) Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar Augustino Shao.
 
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Ali Mohamed Shein akisaini kitabu cha rambirambi
 
 
 

WAZIRI MKUU WA TUNISIA AJIUZULU


Maandamano nchini Tunisia baada ya mauaji ya mwanasiasa wa upinzani Chokri Belaid

Waziri mkuu wa Tunisia Hamadi Jebali, amejiuzulu baada ya kukosa kuafikia makubaliano kuhusu serikali mpya.

Bwana Jebali,alikuwa anajaribu kuunda serikali mpya kufuatia msukosuko wa kisiasa uliosababishwa na mauaji ya mwanasiasa wa upinzani Chokri Belaid wiki mbili zilizopita.

Awali alisema alikuwa tayari kujiuzulu ikiwa chama chake cha kiisilamu cha Ennahda hakingeunga mkono mpango wake wa kuwateua wataalamu kama wanachama wa baraza la mawaziri.

Mauaji ya mwanasiasa huyo yaliyofanyika Februari sita, yalisababisha maandamano na ghasia pamoja na kujiuzulu kwa maafisa wa serikali.

''Niliapa kuwa ikiwa mpango wangu haungefaulu, ningejiuzulu, na nimefanya hivyo,'' alisema bwana Jebali baada ya kukutana na rais Moncef Marzouki. 

Akitaja hatua yake kama jambo la kusikitisha , alisema aliamua kujiuzulu ili kutimiza ahadi yake kwa wananchi wa Tunisia.

"watu wetu wana ndoto fulani, ambazo wanataka wanasiasa kuwatimizia. Laizima tuweze kuwaweka imani watu wetu,'' alisisitiza Jebali.

Na aliongeza kuwa, kukosa kufaulu kwa mpango wangu, haina maana kuwa Tunisia imefeli, au mapinduzi hayakuwa na faida,'' akigusia mapinduzi ya kiraia yaliyofanyika miaka miwili iliyopita ambapo rais wa zamani Zine al-Abidine Ben Ali alipinduliwa.

Tuesday, February 19, 2013

VYAKULA VINAVYOWEZA KUSABABISHA SARATANI


UTAFITI mbalimbali uliokwishafanywa unaonyesha kuwa magonjwa mengi ya saratani (cancer) yanatokana na vyakula tunavyokula kila siku katika maisha yetu. Katika siku za hivi karibuni, ongezeko la magonjwa haya limekuwa kubwa kwa sababau vyakula vinavyosababisha magonjwa hayo, ndivyo vinavyoliwa sana kuliko vile vinavyozuia.

 Wiki iliyopita tuliwaorodheshea baadhi ya vyakula vinavyoaminika kusaidia kuzuia magonjwa ya kansa ambapo wiki hii tunawaletea orodha ya vyakula vinavyoaminika kuongoza kwa kuwa chanzo cha magonjwa hayo hatari:

 

VYAKULA VYA KUKAANGA

 Vyakula vingi vinavyotayarishwa kwa kukaangwa kwenye mafuta yenye moto mkali huwa na madhara kiafya na miongoni ma madhara hayo ni pamoja na kusababisha kansa ya kwenye mfuko wa uzazi. Vyakula hivyo ni pamoja na chips na vyakula vingine vinavyopikwa kwa kukaangwa kwenye mafuta.

 

VYAKULA VYENYE CHUMVI NYINGI

 Vyakula vyenye chumvi nyingi vimebainika navyo kusababisha kansa. Vile vile inaelezwa kuwa chumvi huwa kama chakula kwa bakteria wa kansa tumboni. Kansa ya tumbo inadaiwa kuua watu wengi nchini Japan kutokana na jamii hiyo kupenda sana vyakula vyenye chumvi nyingi. Miongoni mwa vyakula vyenye chumvi nyingi ni vile vya kusindika, kama vile nyama za makopo, maharage,  n.k

 

SUKARI

 Matumizi mabaya ya sukari yanaelezwa kusababisha kansa. Kama tujuavyo, kuna aina mbalimbali za sukari lakini sukari hatari zaidi ni zile zinazowekwa kwenye vinywaji mbalimbali, zikiwemo soda, juisi za ladha ya matunda ambazo huwa na kiwango kingi cha ‘fructose’ ambayo inaelezwa kusababisha saratani ya kongosho.

 Vile vile sukari kwa ujumla wake hairuhusiwi kutumiwa na mtu ambaye tayari amegundulika kuwa na kansa kwa sababu chakula cha chembechembe za saratani mara nyingi huwa ni sukari. Kwa matumizi mengine ya kawaida, sukari inatakiwa kutumiwa kwa kiwango kidogo sana katika vinywaji au vyakula tunavyotumia, tofauti na baadhai ya watu wanavyoweka sukari nyingi ili kupata utamu zaidi.

 

NYAMA ILIYOIVA SANA

 Upikaji wa nyama kwa muda mrefu na kwenye moto mkali (high temperatures) husababisha aina fulani ya kemikali inayojulikana kitaalamu kama ‘heterocyclic aromatic amines’. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Chuo Kikuu cha Utah (University of Utah), umeonesha kwamba watu wanaopenda kula nyama zilizoiva sana, wako hatarini zaidi kupatwa na saratani ya njia ya haja kubwa (Rectal Cancer). Hivyo inashauriwa unapopika nyama, usipike kwenye moto mkali na kuiva kupita kiasi.

POMBE

 Unywaji wa pombe kupita kiasi nao unaelezwa kusababisha aina nyingi ya saratani, kwa wake kwa waume. Aina ya saratani zinazodaiwa kusababishwa na pombe ni pamoja na satarani ya mdomo, ini, utumbo na koromeo, ambazo ndizo zinazoua watu wengi hivi sasa nchini Marekani.

 

NYAMA NA MAFUTA

 Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani, umegundua kwamba watu wanaopenda kula nyama kila siku wako hatarini kupatwa na saratani ya utumbo kuliko wale wanaokula mara moja moja. Pia baadhi ya mafuta ya wanyama na yale yanayowekwa kwenye ‘baga’ au ‘cheese’ huweza kusababisha kansa.

 Vile vile ulaji wa vyakula vilivyotengenezwa kwa kuchanganya na nyama zilizosindikwa au kuhifadhiwa kwa matumizi ya muda mrefu husababisha saratani pia. Vyakula hivyo ni pamoja na ‘soseji’ ambazo hupendwa na watu wengi. Pia mikate ya nyama ‘hot dogs’ nayo ni chanzo cha magonjwa ya saratani.

 

VYAKULA VYA UNGA MWEUPE

Vyakula vyote vinavyopikwa kutokana na unga uliokobolewa na kuondolewa virutubisho vyake vyote na kuwa mweupe, vinaelezwa kuchangia magonjwa ya saratani kwa kiasi kikubwa. Vyakula hivyo ni pamoja na ‘donati’ (doughnuts), maandazi, mkate mweupe, n.k

 Mwisho, licha ya kuepuka ulaji wa vyakula vilivyotajwa hapo juu, unatakiwa kuzingatia ulaji wa vyakula asilia vitokanavyo na mimea, mboga za majani na matunda kwa wingi kila siku. Utaona kwamba adui mkubwa wa afya zetu ni vyakula vyote vya kusindika na vile vya kutengenezwa viwandani au vile ambavyo wakati wa utayarisjaji wake huondolewa virutubisho vyake vya asili.

Monday, February 18, 2013

MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2012 YAMETOKA

 
TAARIFA YA MATOKEO YA MITIHANI YA MAARIFA (QT) NA KIDATO CHA NNE (CSEE)

ILIYOFANYIKA OKTOBA 2012



1.0 UTANGULIZI

Mitihani ya Kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT) kwa mwaka 2012 ilifanyika nchini kote kuanzia tarehe 8-25 Oktoba 2012. Napenda kuchukua nafasi hii kutangaza rasmi matokeo ya mitihani hiyo kama ifuatavyo :



2.0 MTIHANI WA MAARIFA (QT)

2.1 Usajili na Mahudhurio

Katika Mtihani wa Maarifa 2012 watahiniwa waliosajiliwa ni 21,310 ambapo wasichana walikuwa ni 13,134 na wavulana ni 8,176.

Jumla ya watahiniwa 17,137 sawa na asilimia 80.42 ya waliosajiliwa wamefanya Mtihani.



2.2 Matokeo ya Mtihani wa Maarifa (QT)

Watahiniwa 5,984 kati ya 17,137 waliofanya mtihani wamefaulu Mtihani wa Maarifa (QT).



3.0 MTIHANI WA KIDATO CHA NNE (CSEE) 2012

Jumla ya vituo 5,058 vilitumika katika kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 ambapo vituo 4,155 vilikuwa vya watahiniwa wa shule na vituo 903 vilikuwa ni vya watahiniwa wa kujitegemea.


3.1 Usajili na Mahudhurio ya Watahiniwa

(a) Watahiniwa Wote

Jumla ya watahiniwa 480,036 walisajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 wakiwemo wasichana 217,583 sawa na asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67. Watahiniwa waliofanya mtihani wa Kidato cha Nne 2012 ni 456,137 sawa na asilimia 95.44. Watahiniwa 21,820 sawa na asilimia 4.55 ya watahiniwa wote waliosajiliwa hawakufanya mtihani.



(b) Watahiniwa wa Shule

Watahiniwa wa shule waliosajiliwa ni 411,230 wakiwemo wasichana 182,978 sawa na asilimia 44.50 na wavulana 228,252 sawa na asilimia 55.50. Watahiniwa wa shule waliofanya mtihani walikuwa 397,136 sawa na asilimia 96.57. Aidha, watahiniwa 14,090 sawa na asilimia 3.43 hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo utoro, ugonjwa na vifo.

(c) Watahiniwa wa Kujitegemea

Watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa walikuwa ni 68,806 wakiwemo wasichana 34,605 sawa na asilimia 50.29 na wavulana 34,201 sawa na asilimia 49.71. Watahiniwa 61,001 wakiwemo wasichana 30,917 na wavulana 30,084 wamefanya mtihani wakati watahiniwa 7,730 sawa na asilimia 11.23 hawakufanya mtihani.



4.0 MATOKEO YA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE



(a) Watahiniwa wa Shule

Jumla ya watahiniwa wa shule 126,847 kati ya watahiniwa 397,136 waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne 2012 wamefaulu. Wasichana waliofaulu ni 46,161 na wavulana ni 80,686.



(b) Watahiniwa wa Kujitegemea

Idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 16,112 kati ya watahiniwa 61,001 waliofanya mtihani. Wasichana waliofaulu ni 6,751 na wavulana ni 9,361.





5.0 UBORA WA UFAULU KWA MADARAJA NA JINSI

Ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonesha kuwa jumla ya watahiniwa 23,520 wamefaulu katika madaraja I – III ambapo kati yao wasichana ni 7,178 na wavulana ni 16,342.



Mchanganuo wa ufaulu kwa kila Daraja kwa jinsi kwa Watahiniwa wa Shule mwaka 2012 ni kama ifuatavyo:



Idadi ya Wavulana
Idadi ya Wasichana
Jumla
I
1,073
568
1,641
II
4,456
1,997
6,453
III
10,813
4,613
15,426
I-III
16,342
7,178
23,520
IV
64,344
38,983
103,327
0
120,664
120,239
240,903



6.0 SHULE ISHIRINI ZILIZOFANYA VIZURI ZAIDI KATIKA KUNDI LA SHULE ZENYE WATAHINIWA 40 AU ZAIDI

Ubora wa ufaulu wa shule umepangwa kwa kutumia kigezo cha “Grade Point Average” (GPA) kuanzia A = 1 hadi F = 5. Shule zenye watahiniwa 40 na zaidi ziko 3,391. Shule ya kwanza hadi ya ishirini zimeainishwa kwenye Jedwali lifuatalo :

NAFASI
JINA LA SHULE
IDADI YA WATAHINIWA
MKOA
1
ST. FRANCIS GIRLS
90
MBEYA
2
MARIAN BOYS S.S
75
PWANI
3
FEZA BOYS S.S
69
DAR ES SALAAM
4
MARIAN GIRLS S.S
88
PWANI
5
ROSMINI S S
78
TANGA
6
CANOSSA S.S
66
DAR ES SALAAM
7
JUDE MOSHONO S S
51
ARUSHA
8
ST. MARY’S MAZINDE JUU
83
TANGA
9
ANWARITE GIRLS S S
49
KILIMANJARO
10
KIFUNGILO GIRLS S S
86
TANGA
11
FEZA GIRLS
49
DAR ES SALAAM
12
KANDOTO SAYANSI GIRLS SS
124
KILIMANJARO
13
DON BOSCO SEMINARY SS
43
IRINGA
14
ST.JOSEPH MILLENIUM
133
DAR ES SALAAM
15
ST.JOSEPH’S ITERAMBOGO SS
64
KIGOMA
16
ST.JAMES SEMINARY SS
44
KILIMANJARO
17
MZUMBE SS
104
MOROGORO
18
KIBAHA SS
108
PWANI
19
NYEGEZI SEMINARY SS
68
MWANZA
20
TENGERU BOYS SS
76
ARUSHA



7.0 SHULE KUMI AMBAZO HAZIKUFANYA VIZURI ZAIDI KATIKA KUNDI LA SHULE ZENYE WATAHINIWA 40 AU ZAIDI

NAFASI
JINA LA SHULE
IDADI YA WATAHINIWA
MKOA
1
MIBUYUNI S.S
40
LINDI
2
NDAME S.S
41
UNGUJA
3
MAMNDIMKONGO S.S
63
PWANI
4
CHITEKETE S.S
57
MTWARA
5
MAENDELEO S.S
103
DAR ES SALAAM
6
KWAMNDOLWA S.S
89
TANGA
7
UNGULU S.S
62
MOROGORO
8
KIKALE S.S
60
PWANI
9
NKUMBA S.S
152
TANGA
10
TONGONI S.S
56
TANGA



8.0 TATHMINI YA UFAULU WA WATAHINIWA WA MTIHANI WA KIDATO CHA NNE MWAKA 2012

8.1 Tathmini ya awali iliyofanyika kuhusu ufaulu wa watahiniwa katika shule mbalimbali inaonesha kuwa shule zilizofanya vizuri zaidi ni zile ambazo zina mahitaji yote ya msingi ikiwemo walimu wa kutosha, miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Aidha, shule zenye ufaulu wa chini ni zile ambazo zina changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na:

(i) Baadhi ya shule za vijijini hazina kabisa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati na pia zina upungufu mkubwa wa walimu wa masomo mengine;

(ii) Kutokuwepo kwa maabara kwa shule zenye mikondo ya sayansi na pia kutokuwepo kwa maktaba kwa ajili ya kujisomea; na

(iii) Upungufu mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada. Katika baadhi ya shule uwiano wa kitabu kwa mwanafunzi ni 1:10.

8.2 Mkakati wa Serikali ni kuendelea kupunguza changamoto hizo kila mwaka ikiwa ni pamoja na kufanya mambo yafuatayo:

(i) Kuajiri walimu kila mwaka ili kuondoa upungufu uliopo katika shule zetu. Mwaka 2011/2012 Serikali iliajiri walimu wa sekodari 13,246 na mwaka huu wa fedha 2012/2013 imeajiri walimu 12,973 ambao wamepangwa katika shule zenye upungufu mkubwa wa walimu. Ajira ya walimu wapya mwaka huu umetuwezesha kuwa na wastani wa walimu 2-3 kwa shule. Hali hii itaendelea kuboreka kadri tunavyoendela kuajiri walimu.

(ii) Kuboresha miundombinu iliyoko katika shule zetu ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za walimu, madarasa na maabara. Mwaka 2012/2013 Serikali imepanga kuboresha miundombinu katika shule 264 zilizopo katika mazingira magumu ikiwemo miundombinu ya maabara na nyumba za walimu.

(iii) Kuendelea kutoa ruzuku ya Tsh 25,000 kwa mwanafunzi kwa mwaka, ambapo asilimia 50 ya fedha hizo ni kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ili kuziwezesha shule kununua vitabu pamoja na vifaa vingine muhimu kitaaluma.

(iv) Wizara kuendelea kuzishauri Halmashauri kuweka mgawanyo mzuri wa walimu waliopo baina ya shule na shule.

(v) Wizara itaendelea kuimarisha Idara ya Ukaguzi wa Shule pamoja na kuwawezesha Waratibu Elimu Kata na Wakuu wa Shule kufanya ukaguzi wa ndani katika Shule za Sekondari zilizo katika maeneo yao.



9.0 MATOKEO YA MITIHANI YALIYOZUIWA



Baraza la Mitihani la Tanzania limezuia kutoa matokeo ya:

(a) Watahiniwa 28,582 wa Shule ambao hawajalipa ada ya Mtihani hadi watakapolipa ada wanayodaiwa pamoja na faini; na ikiwa hawatalipa katika kipindi cha miaka miwili (02) toka matokeo kutangazwa, matokeo yao yatafutwa.

(b) Watahiniwa 65 wa kujitegemea na 71 waliofanya Mtihani wa Maarifa (QT) mwaka 2012 bila ya kulipa ada ya Mtihani hadi watakapolipa ada pamoja na faini. Ikiwa hawatalipa ada hiyo katika kipindi cha miaka miwili (02) toka matokeo kutangazwa, matokeo yao yatafutwa.



10.0 MATOKEO YA MITIHANI YALIYOFUTWA



10.1 Matokeo Yaliyofutwa Kwa Sababu ya Udanganyifu



Jumla ya watahiniwa 789 wamefutiwa matokeo yao yote ya mtihani kwa mujibu wa kifungu Na.52(b) cha Kanuni za Mitihani baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu katika mitihani ya Oktoba 2012. Kati yao, watahiniwa wa shule ni 624 na watahiniwa wa kujitegema ni 148 na watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa (QT) ni 17.



Aina ya udanganyifu uliobainika na idadi ya watahiniwa husika ni kama ifuatavyo:





S/N
AINA YA UDANGANYIFU
IDADI YA WATAHINIWA
(i)
Watahiniwa kubainika kuwa na skripti zenye miandiko tofauti au kuwa na miandiko tofauti katika skripti ya somo moja au zaidi ya moja.
04
(ii)
Watahiniwa kukamatwa na wasimamizi ndani ya chumba cha mtihani wakiwa na ‘notes.’
170
(iii)
Watahiniwa kubainika kuwa na mfanano usio wa kawaida wa majibu.
590
(iv)
Watu kukamatwa wakiwafanyia watahiniwa wengine mtihani ‘impersonation”.
04
(v)
Watahiniwa kukamatwa na simu ndani ya chumba cha mtihani.
06
(vi)
Watahiniwa kukamatwa na wasimamizi wakibadilisha karatasi za maswali au skripti kwa lengo la kufanya udanganyifu.
15

JUMLA
789



10.2 Matokeo Yaliyofutwa Kwa Sababu ya Watahiniwa Kuandika Matusi Katika Skripti Zao

(i) Jumla ya watahiniwa 24 waliandika matusi kwenye skripti zao za masomo mbalimbali. Kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa kifungu 5(13) cha Kanuni za Mitihani kinachosomeka:

Written responses to any examination question which carry words, drawings or pictures connected to sex or abusive language in such a way that it becomes offensive shall consitute an examination offence and a candidate who commits such an offence shall be punished by the Council.”



Kutokana na kosa hilo Baraza la Mitihani limefuta matokeo yao yote kwa mujibu wa Kifungu cha 6(2)(a) cha Kanuni za Mitihani kinachosomeka:

“A candidate found to have committed an examination offence shall - (a) have his examination results nullified”

(ii) Kitendo cha kuandika matusi kwenye karatasi za majibu (skripti) kinaonesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu. Serikali haitaweza kuwavumilia hata kidogo watahiniwa wa aina hiyo. Hivyo, Serikali itaangalia hatua zaidi za kisheria za kuchukua dhidi ya watahiniwa wote walioandika matusi.

Kwa mujibu wa kifungu Na. 6(2)(b) cha Kanuni za Mitihani, watahiniwa wote waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani au kuandika matusi katika skripti zao hawataruhusiwa kufanya mitihani inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja (01) kuanzia tarehe ya kutangazwa kwa matokeo.



11.0 KUANGALIA MATOKEO YA MTIHANI WA CSEE na QT, 2012



(a) Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT), 2012 yanapatikana katika tovuti zifuatazo:




· www.moe.go.tz



(b) Matokeo yanaweza kupatikana pia kwa njia ya ujumbe mfupi wa maneno (SMS) kwenda namba 15311. Jinsi ya kutuma ujumbe andika:



MATOKEOXNAMBA YA KITUOXNAMBA YA MTAHINIWA

(Mfano : matokeoxS0101x0503)






Dkt. Shukuru Jumanne Kawambwa (Mb)


WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI

18 Februari 2013




KUPATA MATOKEO HAYO BOFYA HAPO CHINI
MATOKEO KIDATO CHA NNE 2012