Polisi nchini Tanzania
wamekamata vipande elfu moja na ishirini na moja vya meno ya tembo vyenye uzito
wa karibu kilo elfu tatu.
Meno hayo ya tembo
yamekamatwa katika bandari ya Zanzibar jana na watu wawili wanashikiliwa kwa
tuhuma za kuhusika na meno hayo. Hata hivyo, bado haijafahamika idadi kamili ya
tembo waliouawa, kwani baadhi ya meno yamekatwa vipande.
Kwa mujibu wa afisa
habari mkuu wa jeshi la polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, kiasi
kilichokamatwa ni kikubwa kuwahi kukamatwa visiwani humo. Kamishna wa Polisi
Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema meno hayo yalikuwa yamehifadhiwa katika
kontena la futi arobaini yakiwa yamechanganywa katika mifuko iliyohifadhi
makombe ya konokono wa baharini, tayari kwa kusafirishwa nje.
Hivi karibuni raia
watatu wa China walikamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na meno 706 ya tembo,
sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.
Kukamatwa kwa meno haya
ya tembo, kumekuja wakati tayari serikali imetangaza kusitisha Operesheni
Tokomeza Ujangili, ambayo ililenga kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka
kutokana na kuuawa katika hifadhi za taifa nchini Tanzania. Wanyama wanaolengwa
zaidi na majangili kutokana na meno yao na pembe ni tembo na faru.
Matukio ya kukamatwa
kwa meno ya tembo kutoka Afrika Mashariki yamekuwa yakiripotiwa kila mara.
Oktoba, 20, 2012, tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya dola milioni 3.4
za Kimarekani yalikamatwa Hong Kong, yakidaiwa kusafirishwa kutoka Kenya na
Tanzania.
Pia Agosti 16 mwaka huu
polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam,
walimkamata raia wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya
shilingi milioni 18 sawa na dola zaidi ya elfu 11, yakisafirishwa kwenda nje.
0 Comment to "ZANZIBAR WAKAMATA MENO YA TEMBO "
Post a Comment