Wednesday, April 30, 2014

ASKARI WANNE NA RAIA 14 WAPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI MKOANI SINGIDA




ASKARI Polisi wanne wa kituo cha Polisi Singida mjini na wakazi 14 wa kijiji cha Utaho tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoani Singida,wamefariki dunia baada ya kugongwa na basi la kampuni ya summry T.799 BET aina ya nissan.

Tukio hilo limetokea Aprili 28 mwaka huu saa 2.45 usiku katika barabara kuu Singida-Dodoma eneo la kijiji cha Utaho wilaya ya Ikungi.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida,SACP.Geofrey Kamwela askari hao ni F.849 D/CPL Boniface Magubika,F.6837 Pc Jumanne Mwakihamba,G.7993 Pc Novatus Tarimo na G.8948 Pc Michael Mwakihaba.
Alitaja wengine waliofariki kuwa ni pamoja na Ramadhani Mjengi afisa mtendaji wa kijiji cha Utaho,Paul Hamisi mwenyekiti wa kijiji cha Utaho,Ernest Salanga,mwenyekiti wa kitongoji cha Utaho,Saidi Rajabu,Usirika Itambu,Chima Mughenyi,Slim Juma,Abeid Ramadhani,Mwinyi Hamisi na Issa Husein wote wakazi wa kijiji cha Utaho.

Aidha.Kamwela amesema kuwa miili ya watu wengine bado haijatambuliwa na imehifadhiwa kwenye chumba cha maiti cha hospitali ya mkoa mjini Singida.

Akizungumuzia juu ya ajali hiyo,kamanda huyo amesema kuwa awali kijana Gerard Zephania (24) akiwa ametoka kusaga nafaka aligongwa na gari la mizigo ambalo bado halijafahamika na kufariki papo hapo.

“Askari wa polisi wakitumia gari PT 1424,walifika eneo la tukio kwa ajili ya kuubeba mwili wa Gerard kuuleta katika hospitali ya mkoa kwa uchunguzi,kundi la wananchi wa kijiji cha Utaho nao walifika eneo la tukio”,amesema na kuongeza;

“Wakati askari polisi wakiwa kwenye harakati ya kuupakia mwili huo ghafla basi la summry liliacha njia na kuingia kushoto mwa barabara kwa nia ya kulikwepa gari la polisi na ndipo lilipovamia na kugonga kundi la watu hao wakiwemo askari polisi.Watu 15 walifariki papo hapo”,amesema Kamwela.
Kamanda Kamwela amesema kuwa dereva wa basi hilo Paulo Njilo mkazi wa Dar-es-salaam hakuweza kusimamisha basi hilo nadi kilomota 25 alipolisimamisha na yeye kutorokea kusikojulikana.

Aidha,amesema ajali hiyo imesababisha majeruhi nane ambapo wawili kati yao wamelazwa katika hospitali ya mkoa na hali zao zinaendelea vizuri.Majeruhi wengine sita wamelazwa katika hospitali ya misioni ya Puma na hali zao sio nzuri.

“Uchunguzi zaidi juu ya ajali hiyo unaendelea ili kujua chanzo halisi cha tukio pamoja na kumtafuta dereva wa basi ili aweze kuhojiwa na kisha hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake”,amesema Kamanda Kamwela.

Wednesday, April 16, 2014

MELI YAZAMA KOREA KUSINI



Meli hiyo ilikuwa na watu 460. Zaidi ya miatatu hawajapatikana , wengine 164 wameokolewa na wengine wawili wamethibitishwa kufariki.

 Meli hiyo ikiwa kwenye muonekano wa kawaida
Meli hiyo ilipoanza kupinduka
Ikiwa imezama imebaki sehemu ya chini kabisa
Waokoaji wakiwa wamewasili eneo la ajali kwa ajili ya kuokoa abiria



Meli ya Korea Kusini iliyokuwa imewabeba zaidi ya abiria mianne sitini ilizama kusini mwa pwani ya nchi hiyo Jumatano asubuh
Zaidi ya watu miatatu bado hawajapatikana baada ya meli iliyokuwa imewabeba wanafunzi kuzama nchini Korea Kusini.

Awali maafisa walikuwa wamesema kuwa wengi wa abiria waliokuwa katika meli hiyo waliokolewa.

Baadhi ya walionusurika wamekuwa wakielezea hali ilivyokuwa ya kutisha ndani ya meli ilipoanza kusimama kwa kuyumba, ikiegemea upande mmoja na haraka kuanza kuzama.

"Kwa kweli kulikuwa na sauti kubwa na meli ghafla ikaanza kuegemea upande mmoja," amesema abiria aliyeokolewa, Kim Song-Muk.

"watu walikuwa wakihangaika kukimbilia maeneo ya juu ya meli, lakini ilikuwa vigumu kufanya hivyo kutokana na meli kupinduka."

Bado haijafahamika kilichosababisha kuzama kwa meli hiyo, ambayo kwa kiasi kikubwa iliwabeba wanafunzi wa shule, lakini watu walionusurika katika ajali hiyo wanatoa maelezo sawa kuhusu tukio hilo la kutisha.

Kikosi cha Walinzi wa Pwani ya Korea Kusini kimesema abiria wapatao mia tatu hawajulikani walipo baada ya meli kupinduka na kuzama.

Watu wawili wamefahamika kupoteza maisha na watu mia moja na sitini na wanne wameokolewa.

Wengi wa abiria wa meli hiyo walikuwa wanafunzi wa sekondari wakiwa katika safari ya masomo kuelekea kisiwa cha Jeju, nchini Korea Kusini.


Tuesday, April 15, 2014

UKRAINE NA RUSSIA WAENDELEZA MVUTANO




Waandamanaji wanaounga mkono Russia hapo Jumatau walikaidi tarehe ya mwisho ya serikali ya kuyaachia majengo walinashikilia  ili wapewe msamaha, huku  kaimu rais wa Ukraine akitishia  kutumia majeshi kuwadhibiti.

Dazeni ya waandamanaji walivunja madirisha kwenye makao makuu ya polisi huko mashariki mwa mji wa Horlivka  na kuwafunga pingu polisi wakati walipochukua udhibiti wa majengo hayo.

Rais wa Marekani Barack Obama alimwonya Rais wa Russia Vladmir Putin katika mazungumzo kwa njia ya simu  Jumatatu  kuwa Moscow itakabiliwa na gharama zaidi ikiwa hatua zake huko Ukraine zitaongezeka.

 Pia alimsihi kiongozi huyo wa Russia kutumia ushawishi wake kuwarai waandamanaji waondoke kwenye majengo wanayoshikilia.  Naye rais Putin alimsihi rais Obama kuiomba serikali ya Ukraine kutotumia nguvu dhidi ya waandamanaji.