Huku ligi kuu soka Tanzania Bara ikiwa imekamilisha mzunguko
wake wa kwanza, timu ya Azam FC ya Dar es Salaam imetangaza kusitisha
mkataba na kocha wake mkuu Stewart Hall wa Uingereza kwa kile kilichoelezwa kama
makubaliano ya pamoja.
Kwa Mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye mtandao wa klabu hiyo jijini Dar es
Salaam, hii itakuwa ni mara ya pili kwa kocha huyo kuachana na klabu ya Azam na
ameafikiana na uongozi wa klabu hiyo baada ya kukamilisha mzunguko wa kwanza wa
ligi hiyo ambapo timu ya Azam sasa inashika nafasi ya Pili baada ya kwenda sare
ya mabao 3-3 na timu ya Mbeya City ambapo zote sasa zina Pointi 27. Bingwa
mtetezi timu ya Yanga inaongoza ligi hiyo kwa sasa ikiwa na pointi 28 baada ya
kuinyuka Oljoro JKT mabao 3-0 katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa
ligi hiyo, maaruf kama Vodacom Premier League.
Klabu ya Azam FC inayoinukia kwa ubora wa miundo mbinu huku ikiendeshwa
kisasa kwa mipango inayoeleweka kinyume na klabu nyingi nchini Tanzania imekuwa
ikifanya vema chini ya mwalimu huyo ambapo msimu uliopita aliiwezesha kushiriki
michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika baada ya kushika nafasi ya Pili
katika Ligi kuu msimu uliopita.
Klabu hiyo inao wachezaji kadhaa wa Kulipwa kutoka nchi za Ivory Coast, Kenya
na Uganda. Kuachia ngazi kwa kocha huyo kunaelezwa kuwa kumekuwa kwa mkakati ili
kusiathiri mwenendo wa timu hususan wakati ligi ikiendelea na sasa kutaiwezesha
Azam FC Kutafuta kocha mwingine hususan wakati huu ambapo ligi imefikia
Mapumziko.
0 Comment to "AZAM FC YAMTIMUA KOCHA"
Post a Comment