Tuesday, February 25, 2014

MUSEVENI ATIA SAINI MSWADA UNAOPINGA MASHOGA



Raia wa Uganda wamekaribisha kutiwa saini kwa mswada unaopinga ushoga na unaopendekeza kifungo cha maisha kwa wale watakaopatikana na hatia. Ni mswada unaoungwa mkono sana na waganda na unaopingwa vikali na mataifa ya magharibi.

Baada ya kuutia saini Rais wa Uganda Yoweri Museveni alisema haelewi ni vipi mwanamme anashindwa kuvutiwa na urembo wa mwanamke na kuvutiwa na mwanamme mwenzake. Aliuza, utawachaje kitu kizuri na kufuata kitu kibaya?
Rais Museveni alisema hangeweza kutia saini mswada dhidi ya mashoga punde tu baada ya bunge kuupitisha mwaka uliopita akisema alitaka kwanza kuelewa kama mashoga wanazaliwa au ni watu wanaoiga tabia isiofaa.

Aliunda jopo la wanasayansi kumshauri kuhusu suala hili jambo lililo-onekana na baadhi ya waganda kana kwamba Rais hakuwa anataka kutia saini mswada huu kwa sababu alikuwa anayaogopa mataifa ya magharibi ambayo yalikuwa yanatishia kusitisha msaada wao ikiwa Rais atatia saini mswada huu.

Rais Museveni alisema Uganda haihitaji misaada kwa sababu misaada hiyo ndiyo chanzo cha  baadhi ya shida ambazo Uganda inazokumbana nazo.

Mbunge David Bahati ndiye aliyeuwasilisha bungeni mswada huu na alisema, “Leo ni ushindi kwa jamii ya Uganda, watu wa Uganda na watoto wa Uganda. Ni ushindi kwa sababu unaonyesha kuwa tuko nchi huru ambayo ilijinyakulia uhuru miaka 50 iliyopita”.

Akitia saini mswada dhidi ya mashoga, Rais Museveni alisema hakuwa anatilia maanani sana suala la mashoga lakini jamii ya kimataifa imekuwa ikimsukuma sana na ndio sababu akaamua kuliangalia kwa makini na amejua kuwa hakuna mtu anayezaliwa akiwa shoga na mataifa ya magharibi yanafaa kukomesha tabia yao ya kuwaambia wa-Afrika wanachofaa kufanya.

Rais wa Marekani Barack Obama alisema alivunjwa moyo na mswada dhidi ya mashoga na akasema ukiwa sheria huenda ukaufanya uhusiano wa Uganda na Marekani kuwa mgumu.

Share this

0 Comment to "MUSEVENI ATIA SAINI MSWADA UNAOPINGA MASHOGA "

Post a Comment