Aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha usalama barabarani, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi (SACP) mstaafu James Kombe amefariki dunia wakati akipatiwa
matibabu katika hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia kifo hicho Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini, Mrakibu
Mwandamizi wa Polisi (SSP) Advera Senso alisema, Kombe alifariki Oktoba 22
mwaka huu na taratibu za mazishi zinaendelea.
Aidha Senso alisema Marehemu Kombe alizaliwa mwaka 1950 huko Mwika mkoani
Kilimanjaro na alijiunga na Jeshi la Polisi tarehe 15 mwezi machi mwaka 1970
baada ya kuhitimu elimu ya sekondari mwaka 1969 nchini Uganda ambapo
alipandishwa vyeo na kupewa madaraka mbalimbali.
Baadhi ya vyeo alivyopitia na miaka ya kupata vyeo hivyo katika mabano ni
pamoja na Sagenti wa Polisi (1973) Mkaguzi Msaidizi wa Polisi (1977), Mkaguzi
wa Polisi (1984), Mrakibu Msaidizi (1986), Mrakibu wa Polisi(1991), Mrakibu
Mwandamizi (1995), Kamishna Msaidizi wa Polisi (1998) na Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Polisi (2002) hadi alipostaafu mwaka 2010.
Baadhi ya nafasi alizowahi kuzitumikia
katika Jeshi la Polisi ni pamoja na kuwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) katika
wilaya za Dodoma, Tarime, Serengeti na Arusha pamoja na Kuwa Mkuu wa Polisi wa
Mkoa (RPC) katika mikoa ya Lindi, Arusha, Kigoma pamoja na Mkuu wa Kikosi cha
Kutuliza ghasia Tanzania na hadi anastaafu alikuwa mkuu wa kikosi cha Usalama
barabarani Tanzania.
0 Comment to "KAMANDA MSTAAFU WA POLISI JAMES KOMBE AFARIKI DUNIA"
Post a Comment