Wakati Rais Jakaya
Kikwete jana akiongoza mamia ya wakazi wa Mkoa wa Iringa na mikoa ya jirani
kwenye mazishi ya aliyekuwa Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, Waziri Mkuu
Mizengo Pinda ameahidi kuwa Serikali itatekeleza ahadi alizotoa jimboni kwake.
Dk Mgimwa, ambaye
alikuwa Mbunge wa Kalenga, alizikwa jana saa 10 jioni katika kijiji cha Magunga
kilichoko Kata ya Maboga mkoani Iringa.
Dk Mgimwa aliyefariki
Januari mosi mwaka huu nchini Afrika Kusini, kutokana na tatizo la figo,
alizikwa katika shamba la makaburi lililopo karibu na nyumbani kwa wazazi wake
katika kijiji hicho.
Akitoa ujumbe wa
Serikali katika mazishi hayo, Pinda alisema wataziangalia ahadi alizotoa
marehemu na kuzifanyia kazi zile ambazo hazijakamilika.
“Katika kumuenzi
marehemu Mgimwa, sisi Serikali tunamuenzi kwa kutekeleza mema yote aliyotuachia,”
aliongeza Pinda.
Pinda alisema Serikali
imepoteza waziri aliyetegemewa katia wizara husika na taifa kwa jumla.
“Zimetolewa sifa nyingi
zikimwelezea Waziri Mgimwa juu ya uaminifu wake. Mimi nimesimama hapa
kuthibitisha hilo, kwa muda mfupi alioteuliwa amefanya kazi kwa uadilifu na
weledi mkubwa na sisi katika Serikali tukasema sasa wizara imempata waziri
anayestahili,” alisema Pinda.
“Kati ya Oktoba 4-15 sisi
serikalini tulimtuma Mgimwa aende Marekani akafanye kazi moja na ndipo
ilipogundulika kuwa alikuwa na tatizo lakini yeye alivumilia hadi kazi
ilipoishi ndipo akarudi na alipofika akasema ngoja aende Afrika Kusini akaangalie
afya yake,” alisema Pinda.
Kwa upande wake, mtoto
wa marehemu Godfrey Mgimwa ambaye alisimama kutoa shukrani kwa Serikali na
wananchi waliofurika katika mazishi hayo, aliiomba Serikali kutekeleza ahadi
kadhaa alizoziacha baba yake kama njia pekee ya kuwafariji wanafamilia na wananchi
wa Jimbo la Kalenga.
“Siku 10 kabla ya
kufariki dunia, baba aliniambia kuwa wakazi wa Jimbo la Kalenga ninawapenda
sana katika kipindi hiki ambacho hali yangu si ya kuridhisha ningependa
niwapelekee mabati 1,200. Ametutoka bila ya kutekeleza ahadi hiyo, watoto na
wanafamilia tunaomba Serikali kutekeleza ahadi hizo kama njia pekee ya
kutufariji,” alisema Godfrey.
Godfrey alitaja miradi
minne ambayo baba yake alimweleza kuwa alikuwa anataka kuwatekelezea wakazi wa
jimbo hilo kuwa ni pamoja na umeme, minara ya simu, uanzishaji wa ushirika wa
kuweka na kukopa na barabara.
Akitoa mahubiri yake
katika ibada ya misa ya mazishi ya marehemu Mgimwa, Msaidizi wa Makamu wa
Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Iringa, Padri Julius Kingalawe, alisema
taifa limefikia hatua mbaya ya watu kutokuaminiana.
0 Comment to "SERIKALI KUTEKELEZA AHADI ZA MGIMWA JIMBONI KWAKE"
Post a Comment