Jumuiya ya
Taasisi za kidini za Kiislamu nchini Tanzania imeitaka serikali kufanya
uchunguzi wa kina ili kubaini na kuwachukulia hatua watu waliompiga risasi
Sheikh Ponda Issa Ponda Jumamosi mjini Morogoro, Mashariki mwa nchi hiyo.
Kwa
mujibu wa mwandishi wa wetu, sheikh huyo ambaye amekuwa katika mivutano ya mara
kwa mara na serikali ya Tanzania alipigwa risasi baada ya kutokea vurugu kwenye
mkutano wa mawaidha ya baraza la sikukuu ya Idd el Fitr.
Mwenyekiti
wa Jumuiya hiyo, Alhajj Mussa Kundecha, amewaambia waandishi wa habari mjini
humo kuwa endapo serikali haitachukua hatua itakayowaridhisha Waislamu,
wataamua kufikiria upya mustakabali wao na serikali ya Tanzania.
Sheikh
Ponda amelazwa katika hospitali ya taifa, Muhimbili, mjini Dar es Salaam
akiuguza jeraha la risasi huku akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu.
Msemaji
wa Jeshi la polisi nchini humo Advera Senso amesema kuwa jeshi lake kwa
kushirikiana na jukwaa la haki jinai wameunda kikosi kazi kwa ajili ya kufanya
uchunguzi wa tukio hilo huku akikana kuwa Sheikh Ponda hakupigwa risasi na
polisi.
Senso
amewalaumu wafuasi wa Sheikh Ponda kwa kuwazuia askari kumkamata Sheikh huyo
kwa kuwarushia mawe; hatua iliyosababisha askari hao kufyatua risasi hewani ili
kuwatawanya na hata hivyo wafuasi hao walifanikiwa kumtorosha kiongozi huyo wa
kidini.
Taarifa
za jumuiya hiyo ambayo inajulikana zaidi Tanzania kama Sura ya Maimamu zinasema
kuwa Sheikh Ponda ambaye polisi wanasema walikuwa wakimtafuta kwa tuhuma za
kutoa matamko ya uchochezi, alisafirishwa usiku kutoka mji wa Morogoro hadi Dar
es Salaam zaidi ya kilomita 200.
Sheikh
Ponda kwa sasa anatumikia kifungo cha nje cha mwaka mmoja alichohukumiwa mapema
mwaka huu baada ya kukutwa na makosa kadhaa ikiwemo uchochezi wa kuharibu mali
za watu.
0 Comment to "SHEIKH PONDA ALINDWA HOSPITALINI "
Post a Comment