ASKARI
Polisi wanne wa kituo cha Polisi Singida mjini na wakazi 14 wa kijiji cha Utaho
tarafa ya Ihanja wilaya ya Ikungi mkoani Singida,wamefariki dunia baada ya
kugongwa na basi la kampuni ya summry T.799 BET aina ya nissan.
Tukio
hilo limetokea Aprili 28 mwaka huu saa 2.45 usiku katika barabara kuu
Singida-Dodoma eneo la kijiji cha Utaho wilaya ya Ikungi.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida,SACP.Geofrey Kamwela askari hao ni
F.849 D/CPL Boniface Magubika,F.6837 Pc Jumanne Mwakihamba,G.7993 Pc Novatus
Tarimo na G.8948 Pc Michael Mwakihaba.
Alitaja
wengine waliofariki kuwa ni pamoja na Ramadhani Mjengi afisa mtendaji wa kijiji
cha Utaho,Paul Hamisi mwenyekiti wa kijiji cha Utaho,Ernest Salanga,mwenyekiti
wa kitongoji cha Utaho,Saidi Rajabu,Usirika Itambu,Chima Mughenyi,Slim
Juma,Abeid Ramadhani,Mwinyi Hamisi na Issa Husein wote wakazi wa kijiji cha
Utaho.
Aidha.Kamwela
amesema kuwa miili ya watu wengine bado haijatambuliwa na imehifadhiwa kwenye
chumba cha maiti cha hospitali ya mkoa mjini Singida.
Akizungumuzia
juu ya ajali hiyo,kamanda huyo amesema kuwa awali kijana Gerard Zephania (24)
akiwa ametoka kusaga nafaka aligongwa na gari la mizigo ambalo bado
halijafahamika na kufariki papo hapo.
“Askari
wa polisi wakitumia gari PT 1424,walifika eneo la tukio kwa ajili ya kuubeba
mwili wa Gerard kuuleta katika hospitali ya mkoa kwa uchunguzi,kundi la
wananchi wa kijiji cha Utaho nao walifika eneo la tukio”,amesema na kuongeza;
“Wakati
askari polisi wakiwa kwenye harakati ya kuupakia mwili huo ghafla basi la
summry liliacha njia na kuingia kushoto mwa barabara kwa nia ya kulikwepa gari
la polisi na ndipo lilipovamia na kugonga kundi la watu hao wakiwemo askari
polisi.Watu 15 walifariki papo hapo”,amesema Kamwela.
Kamanda
Kamwela amesema kuwa dereva wa basi hilo Paulo Njilo mkazi wa Dar-es-salaam
hakuweza kusimamisha basi hilo nadi kilomota 25 alipolisimamisha na yeye
kutorokea kusikojulikana.
Aidha,amesema
ajali hiyo imesababisha majeruhi nane ambapo wawili kati yao wamelazwa katika
hospitali ya mkoa na hali zao zinaendelea vizuri.Majeruhi wengine sita
wamelazwa katika hospitali ya misioni ya Puma na hali zao sio nzuri.
“Uchunguzi
zaidi juu ya ajali hiyo unaendelea ili kujua chanzo halisi cha tukio pamoja na
kumtafuta dereva wa basi ili aweze kuhojiwa na kisha hatua za kisheria ziweze
kuchukuliwa dhidi yake”,amesema Kamanda Kamwela.
0 Comment to "ASKARI WANNE NA RAIA 14 WAPOTEZA MAISHA KATIKA AJALI MKOANI SINGIDA"
Post a Comment