Kocha Mkuu wa klabu ya Yanga, Ernest Brandts amesema
timu yake itafanya vizuri katika mechi ya marudiano ya kirafiki dhidi ya Black
Leopards ya Afrika Kusini niliyopangwa kufanyika mapema jioni ya leo ndani ya
uwanja wa CCM-Kirumba mjini Mwanza.
Brandts alisema wachezaji wake wote wamefikia
kiwango kile anachotaka na mchezo huo utakuwa muhimu sana kwake kwani ni wa
mwisho kabla ya kuingia katika kampeni za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania
Bara.
Alisema kuwa Black Leopards ni timu nzuri na
walipata mazoezi mazuri katika mechi ya kwanza iliyofanyika kwenye uwanja
waTaifa jijini na kushinda kwa mabao 3-2.
“Ni mechi nzuri ambayo nadhani itakuwa ni kipimo
kikubwa kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, wachezaji wangu wana
viwango vizuri sana kwa sasa na naamini makosa yaliyofanyika katika mechi ya
kwanza hawatayafanya tena,” alisema Brandts.
Msemaji wa Klabu Yanga, Baraka Kizuguto alisema jana
kuwa pamoja na mechi hiyo kuwa ya maandalizi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara, pia
wameamua kuicheza ili kuwapa burudani mashabiki wa Mwanza.
Kizuguto alisema kuwa Yanga haitakuwa na mechi
yoyote katika mzunguko wa pili Kanda ya ziwa na hiyo ndiyo nafasi yao ya
kuwaonesha uwezo wao mkubwa mashabiki wa Mwanza nini wamekipata kutoka
Uturuki.
“Tuna mashabiki wengi sana Mwanza na Kanda ya Ziwa
kwa ujumla, hii ni fursa kwetu kwani mahsbaiki na wanachama watapata fursa ya
kuona kiwango na maandalizi ya timu yao kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili,”
alisema Kizuguto.
0 Comment to "YANGA KUCHEZA TENA LEO NA BLACK LEOPARDS CCM KIRUMBA MWANZA LEO"
Post a Comment