Sunday, June 16, 2013

TAIFA STARS YAFUNGWA NA IVORY COAST 4 - 2


Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imefungwa mabao 4-2 dhidi ya Ivory Coast na kuzima harakati zake za kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014 huko Brazil. 

Watanzania wengi na wadau wa michezo walidhani Taifa Stars ingeweza kusonga mbele katika harakati hizo za kufuzu kucheza Kombe la Dunia 2014, lakini sasa ukweli umejidhihirisha.

Sasa wengi wamekubaliana na uhalisia wa mambo kwamba, inahitaji muda kidogo kuona Taifa Stars ikisonga mbele katika kuelekea kufuzu Kombe la Dunia na siyo rahisi kama ilivyodhaniwa hapo kabla.

Ni mambo mengi yaliyotokea katika mchezo dhidi ya Ivory Coast ambayo yaliigharimu Taifa Stars licha ya uwanja kujaa idadi kubwa ya mashabiki waliokuwa wakiishangilia timu yao bila kuchoka.

Jambo la msingi ni kwamba, Taifa Stars ikiwa katika harakati za kuhakikisha inafuzu Kombe la Dunia wengi tulisahau kwamba, kwa ‘reality’ ilikuwa ngumu kwa Taifa Stars kufuzu fainali hizo japokuwa kwa mapenzi tulidhani timu hii ingeweza kufuzu kwa kuanza na vipigo kwa timu za Morocco na Ivory Coast.

Tukitazama mchezo kati ya Taifa Stars na Ivory Coast kuna baadhi ya mambo yalionekana kwamba bado tuna safari ndefu ya kufuzu Kombe la Dunia kama kweli tuna nia ya kufanya hivyo.

Mambo mengi mno yalijitokeza katika mchezo kati ya Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast na haya ni machache kati ya mengi yake;

Safu ya Ulinzi Ilipaparika; Ilikuwa kama kila mchezaji ameahidiwa kiasi kikubwa cha fedha, kwani mara nyingi wachezaji wa Taifa Stars hawakucheza katika nafasi zao na hilo liligharimu timu na kujikuta wakilala mabao 4-2.

Erasto Nyoni ndiye beki anayeweza kuondoka na lawama nyingi lakini halikuwa kosa lake wakati mwingine kwani alilazimika kwenda katikati kusahihisha makosa ya mabeki wa kati na kuisahau nafasi yake.

Ilionekana wazi kwamba yalikuwepo mawasiliano hafifu juu ya kutengeneza mtego wa kuotea yaani ‘offside trick’ na matokeo yake Ivory Coast walitumia vyema mwanya huo na kujipatia mabao manne.
Baada ya kuonekana ‘njia’ tangu dakika za mwanzo, beki Erasto Nyoni inaonekana hakupata ushauri wa kutosha kuhusu kutulia na kucheza soka kwani hata makelele ya mashabiki yalimfanya aonekane mtu asiyefaa kikosini. Lakini alikuwepo benchi anayeweza kumudu nafasi yake moja kwa moja?

Nguvu hafifu; Wachezaji wengi wa Taifa Stars walionekana kutokuwa na nguvu ya kupambana na wenzao wa Ivory Coast kutokana na hali halisi ya miili yao.
Sure Boy mfupi na mwenye mwili mdogo alionekana kama mchezaji wa kawaida mbele ya Yaya Toure mwenye mwili mkubwa na nguvu, na mara nyingi Toure aliiwahi mipira ambayo ingeweza kuwahiwa na Sure Boy.

Domayo naye hakuweza kufua dafu mbele ya Traore Lucina na Jean Jacques ambao wote ni watu wa miraba minne. 


Kikosi cha Ivory Coast

Share this

Artikel Terkait

0 Comment to "TAIFA STARS YAFUNGWA NA IVORY COAST 4 - 2"

Post a Comment