Tanzania na mataifa
jirani ya Afrika Mashariki yanatajwa kuwa yanaweza kuboresha pato la ndani la
mwaka – GDP – kama yatachukua hatua za kuboresha ubora wa bandari ya Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa ripoti
mpya iliyopewa kichwa cha ‘Opening the Gates: How the port of Dar es Salaam can
transform Tanzania’ iliyoandikwa na Jacques Morisset, mchumi mkuu wa Benki ya
Dunia kwa Tanzania, Uganda na Burundi, Tanzania na majirani zake wanaweza
kuongeza pato lao la ndani kwa kiwango kikubwa.
Ripoti hiyo inasema
Tanzania inaweza kuongeza pato lake la ndani kwa kiasi cha dola bilioni
1.8 na nchi jirani zinaweza kupandisha
pato la ndani kwa dola milioni 830 kwa mwaka, kiwango ambacho kinaelezewa ni
hasara iliyotokea mwaka 2012.
Ripoti hiyo inasema
kuwa bandari ya Dar es Salaam iko katika njia kuu ya biashara ya Tanzania kwa
asilimia 90, na inashughulikia bidhaa zinazogharimu dola bilioni 15 kwa mwaka,
sawa na asilimia 60 ya pato la ndani la Tanzania kwa mwaka 2012.
Bandari hiyo pia
inaelezewa kuwa inatumiwa na majirani sita wa Tanzania, ambao nchi zao hazina
bandari, nchi hizo ni Malawi, Zambia, Burundi, Rwanda, Uganda na mashariki mwa
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.
Mwaka 2012 pekee,
ripoti inasema hasara ya jumla inayoelezewa ambayo imetokea katika bandari hiyo
imefikia dola bilioni 1.8 kwa uchumi wa Tanzania na dola milioni 830 kwa nchi
jirani. Hasara ambayo ni sawa na asilimia saba ya pato la ndani la mwaka la
Tanzania, na kwa kiasi kikubwa imeathiri wanunuzi wa ndani, biashara na
mashirika ya serikali.
Moja ya sababu ambazo
inaelezewa zimechangia katika hasara hii ni utendaji mbaya wa bandari ya Dar es
Salaam ambao umezigharimu nchi nyingine jirani nazo kupata hasara, na hivyo
kulazimika kulipa fedha zaidi kwa bidhaa zinazoagiwa kutoka nje, ikiwemo bidhaa
za msingi kama vile mafuta ghafi, simenti, mbolea na madawa.
Moja ya vigezo vilivyoelezewa katika ripoti ambavyo
vinachangia katika kusababisha hasara ni
pamoja na uchelewesho unaozikabili meli ambazo zinafika katika bandari ya Dar
es Salaam. Katikati ya mwaka 2012, meli
zilisubiri kwa takriban siku 10 ili kuweza kuruhusiwa kutia nagan na siku 10
nyingine za ziada ili kuweza kushusha mizigo.
Rushwa pia imetajwa
kuwa ni kigezo kingine kinachochangia katika utendaji mbaya wa Bandar, kama
chanzo cha utendaji mbaya na kusababisha hasara kubwa.
0 Comment to "BANDARI YA DAR ES SALAAM NI KICHOCHEO CHA UCHUMI – BENKI YA DUNIA"
Post a Comment