Idadi ya watahiniwa
waliofaulu mtihani wa kidato cha nne mwaka jana imeongezeka kwa kati ya
asilimia 20 na 23 baada ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), kufanya
marekebisho alama za viwango vya ufaulu, Mwananchi limebaini.
Habari ambazo gazeti
hili imezipata zinasema matokeo hayo ambayo yamewezesha kiwango cha ufaulu
kupanda na kufikia asilimia kati ya 54 na 57, huenda yakatangazwa wiki hii
pamoja na yale ya kidato cha sita ambayo pia yamechelewa kutangazwa.
Chanzo cha habari
kutoka Necta kimesema matokeo hayo mapya yanaonyesha kuwa, ufaulu wa kuanzia
daraja la kwanza hadi la nne umeongezeka kutoka asilimia 34.5 kwa matokeo
yaliyotangazwa awali na huenda yakafikia asilimia 57. Hii inamaanisha kwamba
watahiniwa wapatao 82,000 ambao awali walikuwa wamepata sifuri katika matokeo
ya awali sasa wamepanda na kupata madaraja ya ufaulu katika matokeo mapya.
Kwa matokeo hayo,
watahiniwa wa mwaka 2012 watakuwa wamefanya vizuri kuliko wa mwaka 2011, ambao
watahiniwa 225,126 sawa na asilimia 53.37 ya 349,390 waliofanya mtihani huo
walifaulu.
Msemaji wa Necta, John
Nchimbi alisema upangaji wa matokeo hayo ulikuwa bado unaendelea. “Ninachojua
kwa sasa ni kuwa mchakato unaendelea na matokeo yatatangazwa mapema tu ili
watoto waweze kujiunga na shule mapema,” alisema Nchimbi.
Pia alisema
usahihishaji wa mitihani ya kidato cha sita umekamilika.
Matokeo ya awali
Matokeo ya awali
yaliyotangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa
yalionyesha kuwa kati ya watahiniwa 367,756 waliofanya mtihani wa kidato cha
nne mwaka jana, waliokuwa wamefaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu walikuwa
126,847 sawa na asilimia 6.4. Waliopata daraja la nne walikuwa ni 103,327 sawa
na asilimia 28.1.
Katika matokeo hayo,
watahiniwa 240,909 sawa na asilimia 65.5 walipata sifuri, hesabu ambayo
imebadilika katika matokeo mapya ambayo yanaonyesha kuwa sasa waliopata daraja
hilo ni 158,100 ambayo ni asilimia 43.
Hata hivyo, habari
kutoka Necta zinasema kuwa licha ya kuwezesha kuongezeka kwa waliofaulu,
matumizi ya kanuni mpya ya kukokotoa matokeo hayo yalisababisha zaidi ya
wanafunzi 2,500 kushuka ufaulu ikilinganishwa na awali.
Maofisa mbalimbali wa
Necta pamoja na wale wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na taasisi zake,
walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita kukubaliana masuala mbalimbali juu ya
matokeo hayo pamoja na suala la matokeo ya wanafunzi hao 2,500 kabla ya
kutangazwa wiki hii.
“Baada ya wajumbe
kujadili suala lile, busara ilibidi itumike kwa hiyo hakuna mwanafunzi ambaye
alama yake itashuka, kwa kawaida isingewezekana mtoto ambaye matokeo yalitoka
akiwa amefaulu leo umwambie ameshuka,” kilieleza chanzo chetu.
Matokeo ya awali ndiyo
chimbuko la kupitiwa upya baada ya wadau kuyalalamikia na kumlazimisha Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda kuunda tume ya kuyachunguza Februari 23, mwaka huu.
Kabla ya tume hiyo
kuhitimisha shughuli zake, ilitoa taarifa ya awali ambayo ilipendekeza kufutwa
kwa matokeo hayo kwa maelezo kwamba Necta ilitumia kanuni mpya ya kukokotoa
matokeo bila kushauriana na wadau.
Serikali ilitoa taarifa
bungeni kwamba imeamua kufuta matokeo ya 2012 na kuamuru yapangwe upya kwa
kufuata madaraja yaliyotumika mwaka 2011.
0 Comment to "NEEMA KWA WALIOFELI KIDATO CHA NNE"
Post a Comment