Tuesday, May 7, 2013

DAVID CAMERON: "SOMALIA IMEPIGA HATUA"



Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron amesema kuwa Somalia "imepiga hatua kubwa" katika kumaliza fujo na machafuko yaliodumu kwa zaidi ya miongo miwili.
 
Bwana Cameron ni mwenyeji wa mkutano wa kutafuta amani ya kudumu nchini Somalia.
 
Mkutano huo unalengo la kumsaidia Rais Hassan Sheikh Mohamud aweze kuijenga tena upya Somalia.
 
Somalia inahesabiwa kuwa miongoni mwa mataifa yalioanguka na ambayo imekuwa ikihangaishwa na magaidi wa Al shabaab, uharamia na ukame ulioitikisa mwaka kati ya 2010 hadi 2012.
Rais Mohamud wa Somalia amesema serikali yake itafaulu kuidhibiti nchi nzima na kukabiliana na utovu wa usalama ifikapo mwaka 2015.
 
Mkutano huo utajikita zaidi katika masuala ya kujenga upya vikosi vya ulinzi na kukabiliana na ubakaji ambalo ni suala linalooonekana kama mwiko.
 
Takriban watu saba waliuawa katika mlipuko wa bomu kwenye gari uliotokea katika mji mkuu Mogadishu siku ya Jumapili. Kundi la Al - Shabab ambalo lina mafungamano na Al - Qaeda linadai kuhusika na shambulio hilo.
 
Mkutano huo ambao utakua chini ya uenyekiti wa Bw. Cameron na rais wa Somalia Hassan Sheikh Mahamoud unafuatia mkutano kama huo uliofanyika London na jijini Istanbul nchini uturuki mwaka jana, huku wasiwasi ukiongezeka katika jumuiya ya kimataifa kwamba Somalia imegeuka hifadhi ya wanamgambo wenye mahusiano na al Qaeda.
"Ninamatumaini kwamba, wote tunaweza kuafikiana kuhusu mpango wa usalama wa muda mrefu, ambao utamaliza vitisho vya Al Shabab moja kwa moja," alisema Bw. Cameron.
 
"Pia ninamatumaini tutaboresha uwazi na uwajibikaji ili watu wafahamu wapi rasilimali zinakwenda. Pia tunahitaji kuendelea na mchakato wa kulijenga taifa la Somalia, ikiwemo mikoa yote ya Somalia na nchi jirani hali kadhalika."
 
Mchambuzi wa masuala ya Somalia wa BBC, Mary Harper anasema, kumekuwa na mabadiliko ya ghafla nchini humo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
 
Kuna serikali mpya, ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili kutambuliwa na Marekani, Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na wadau wengine muhimu, anasema.

 



 








Share this

Artikel Terkait

0 Comment to "DAVID CAMERON: "SOMALIA IMEPIGA HATUA""

Post a Comment