Wanasheria wa rais
mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta, wameiomba Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya
Jinai, ICC, kumfutia mashitaka yanayomkabili mbele ya mahakama hiyo.
Bwana Kenyatta
amekanusha kuchochea ghasia baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.
Kikao maalum cha
mahakama hiyo kimefanyika wiki moja baada ya mashitaka dhidi ya
mshtakiwa-mwenza, Francis Muthaura, kutupiliwa mbali na mahakama ya ICC.
Mawakili wa Kenyatta
wanasema kuachiwa kwa Muthaura, pia kunafuta mashitaka dhidi ya Kenyatta,
lakini mwendesha mashitaka wa ICC amesema ana ushahidi zaidi dhidi ya Uhuru
Kenyatta.
Kesi dhidi ya Bwana
Kenyatta, ambaye alishinda uchaguzi mkuu uliofanyika mapema mwezi huu, na
kutangazwa rais mteule baada ya kupata asilimia kidogo juu ya 50%, imepangwa
kuanza kusikilizwa mwezi Julai.
Baada ya matokeo ya
uchaguzi wa Desemba mwaka 2007 - wakati Bwana Raila Odinga aliposhindwa dhidi
ya Rais wa sasa Mwai Kibaki, zaidi ya watu 1,000 waliuawa na wengine 600,000
kuachwa bila makaazi.
Bwana Kenyatta, mtoto
wa mwasisi wa taifa la Kenya, Jomo Kenyatta anatuhumiwa kupanga mashambulio
dhidi ya makundi ya kikabila yaliyokuwa yakimuunga mkono Bwana Odinga kufuatia
uchaguzi wa mwaka 2007.
Shahidi muhimu
'haaminiki'Zaidi ya Wakenya 1,000 waliuawa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007.
Wiki iliyopita, mwendesha mashitaka wa ICC, Fatou Bensouda alisema kesi dhidi
ya Bwana Muthaura imetupiliwa mbali kufuatia baadhi ya mashahidi kuogopa kutoa
ushahidi wao, huku mwingien akikana sehemu ya ushahidi wake na kukiri kupokea
rushwa.
Shahidi muhimu -
akijulikana kama shahidi namba nne - alikuwepo katika mkutano ambako
BwanaMuthaura na Bwana Kenyatta walituhumiwa kupanga kuwatumia kikundi cha
Mungiki kinachoogopewa nchini humo kuwashambulia Wakalenjin, ambao walionekana
kuwa wafuasi wa Bwana Odinga katika uchaguzi wa mwaka 2007.
Kiongozi wa mawakili wa
Bwana Kenyatta, Stephen Kay anesema kwa kuwa shahidi namba nne ndiye
aliyemhusisha Kenyatta na kikundi cha Mungiki, kwa hiyo kujitoa kwake katika
ushahidi kuna maana kwamba Kenyatta hana kesi ya kujibu.
"kwa kiasi fulani
tumepoteza imani katika utoaji maamuzi kama tulivyotahadharisha kikao cha
kwanza cha mahakama cha kuthibitisha mashitaka, kutokana na aina ya ushahidi
uliokuwa ukitolewa , na tukapuuzwa," Bwana Kay tameiambia mahakama ya ICC,
ripoti kutoka shirika la AFP.
"Ushahidi dhidi ya
Bwana Muthaura ambao umelazimisha kuondolewa kwa mashitaka dhidi ya Kenyatta ni
sawa sawa na Bwana Kenyatta," amesema.
Amewaomba majaji
kurejesha kesi ya Bwana Kenyatta kwenye mahakama ya kuthibitisha kesi ili
majaji waweze kupitia ushahidi uliobakia kabla ya kuanza kesi kusikilizwa na
kuamua kama kuna ushahidi kamili unaothibitisha kesi hiyo kusikilizwa.
Mwandishi wa BBC Anna
Holligan kutoka The Hague anasema baada ya kufutwa kwa kesi dhidi ya mtuhumiwa
mwenzake, Francis Muthaura, kumekuwa na uvumi kwamba mashitaka dhidi ya Bwana
Kenyatta huenda pia ikatupiliwa mbali.
0 Comment to "UHURU ATAKA MASHTAKA YAKE ICC YAFUTWE"
Post a Comment