Baadhi ya wachimba migodi walioachiliwa na polisi kufuatia ghasia nchini Afrika Kusini
Takriban wachimba migodi 15,000 nchini Afrika Kusini ambao nusura wafutwe kazi kwa kushiriki mgomo haramu, wamerejea kazini.
Kwa mujibu wa kampuni ya Gold Fields, mwajiri wao, takriban wachimba migodi 1,500 ambao hawakurejea kazini siku ya Alhamisi wamefutwa kazi.
Sekta ya madini nchini humo, ambayo ni mojawapo ya kubwa zaidi duniani, imekumbwa na migomo katika wiki za hivi karibuni ambapo takriban wachimba migodi 50 wameuawa.
Vurugu migodini zimeathiri pakubwa uchumi wa nchi hiyo na hata kusababisha sarafu ya Rand kupoteza thamani.
Katika juhudi za kumaliza mgogoro huo, Rais Jacob Zuma wiki hii aliwataka wachimba migodi kurejea kazini na kuwataka wenye makampuni kutopokea mishahara angalau kwa mwaka mmoja ili kunusuru uchumi wa nchi.
Kampuni ya Gold Fields inasema kuwa wachimba migodi 11,000 walirejea kazini siku ya Ijumaa.
Imeongeza kuwa wafanyakazi 2,800 katika mgodi wa Beatrix walirejea kazini siku ya Alhamisi.
Kampuni nyingine ya Anglo American Platinum (Amplats) - ambayo ndiyo kubwa zaidi katika uzalishaji wa madini ya Platinum, wiki jana iliwafuta kazi wafanyakazi 12,000 waliokuwa wanagoma.
Siku ya Jumanne Polisi waliwakamata wachimba migodi 40 waliokuwa wanagoma na ambao waliiba vifaa vya kampuni ya Anglo American vyenye thamani ya mamilioni ya dola katika mkoa wa Northern Cape.
Rais Jacob Zuma ameunda tume ya majaji kuchunguza mauaji ya watu 44 katika mgodi wa Marikana, 34 kati yao waliuawa na polisi.
Uchunguzi huo utabaini ikiwa polisi, wakuu wa makampuni vyama vya wafanyakazi na Serikali walihusika na mauaji hayo.
0 Comment to "WACHIMBA MIGODI WAREJEA KAZINI A.KUSINI"
Post a Comment