MELI ya Mv Victoria
inayomilikiwa na Kampuni ya huduma za Meli nchini (MSC) imenusurika kuteketea
kwa moto uliozuka wakati mafundi wa kampuni hiyo wakichomelea eneo la shimo la
kuhifadhia mizigo la mojawapo ya maeneo kwenye Meli hiyo. Moto huo
uliozuka katika meli hiyo ulizua tafrani kwa wakazi wa jiji la Mwanza na
kufurika katika eneo la maegesho ya Meli za Kampuni ya MSC yaliyopo katika
bandari ya Mwanza
Maafisa wa kikosi cha kuzima moto
walijitosa kuhakikisha moto huo hausambai katika maeneo mengine ya Meli ya Mv
Victoria ambapo walifanikiwa kuuzima huku ukiwa tayari umeteketeza magodoro yote
pamoja na mito ya makochi iliyokuwa katika chumba cha kuhifadhia mizigo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizo naswa toka
kwa wafanyakazi wa Meli hiyo ambao hawakutoa ushirikiano kuzungumza na waandishi
wa habari, zilizonaswa wakati wakilaumiana zimeleeza kuwa mafundi wa kampuni
hiyo walikuwa wakichomelea katika moja ya vyumba vya chini vya Meli hiyo ndipo
cheche za moto zilipopenya na kuangukia katika sehemu ya pili ya kuhifadhia
mizigo na kuanza kuwaka. Sehemu hiyo ya mizigo kulikuwa kumehifadhiwa shehena ya
magodoro pamoja na mito ya makochi tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda mjini
Bukoba Mkoani Kagera
0 Comment to "MELI YA MV VICTORIA YANUSURIKA KUTEKETEA KWA MOTO"
Post a Comment