UTAFITI mbalimbali
uliokwishafanywa unaonyesha kuwa magonjwa mengi ya saratani (cancer) yanatokana
na vyakula tunavyokula kila siku katika maisha yetu. Katika siku za hivi
karibuni, ongezeko la magonjwa haya limekuwa kubwa kwa sababau vyakula
vinavyosababisha magonjwa hayo, ndivyo vinavyoliwa sana kuliko vile
vinavyozuia.
Wiki iliyopita tuliwaorodheshea baadhi ya
vyakula vinavyoaminika kusaidia kuzuia magonjwa ya kansa ambapo wiki hii
tunawaletea orodha ya vyakula vinavyoaminika kuongoza kwa kuwa chanzo cha
magonjwa hayo hatari:
VYAKULA VYA KUKAANGA
Vyakula vingi vinavyotayarishwa kwa kukaangwa
kwenye mafuta yenye moto mkali huwa na madhara kiafya na miongoni ma madhara
hayo ni pamoja na kusababisha kansa ya kwenye mfuko wa uzazi. Vyakula hivyo ni
pamoja na chips na vyakula vingine vinavyopikwa kwa kukaangwa kwenye mafuta.
VYAKULA VYENYE CHUMVI
NYINGI
Vyakula vyenye chumvi nyingi vimebainika navyo
kusababisha kansa. Vile vile inaelezwa kuwa chumvi huwa kama chakula kwa
bakteria wa kansa tumboni. Kansa ya tumbo inadaiwa kuua watu wengi nchini Japan
kutokana na jamii hiyo kupenda sana vyakula vyenye chumvi nyingi. Miongoni mwa
vyakula vyenye chumvi nyingi ni vile vya kusindika, kama vile nyama za makopo,
maharage, n.k
SUKARI
Matumizi mabaya ya sukari yanaelezwa
kusababisha kansa. Kama tujuavyo, kuna aina mbalimbali za sukari lakini sukari
hatari zaidi ni zile zinazowekwa kwenye vinywaji mbalimbali, zikiwemo soda,
juisi za ladha ya matunda ambazo huwa na kiwango kingi cha ‘fructose’ ambayo
inaelezwa kusababisha saratani ya kongosho.
Vile vile sukari kwa ujumla wake hairuhusiwi
kutumiwa na mtu ambaye tayari amegundulika kuwa na kansa kwa sababu chakula cha
chembechembe za saratani mara nyingi huwa ni sukari. Kwa matumizi mengine ya
kawaida, sukari inatakiwa kutumiwa kwa kiwango kidogo sana katika vinywaji au
vyakula tunavyotumia, tofauti na baadhai ya watu wanavyoweka sukari nyingi ili
kupata utamu zaidi.
NYAMA ILIYOIVA SANA
Upikaji wa nyama kwa muda mrefu na kwenye moto
mkali (high temperatures) husababisha aina fulani ya kemikali inayojulikana
kitaalamu kama ‘heterocyclic aromatic amines’. Utafiti wa hivi karibuni
uliofanywa na Chuo Kikuu cha Utah (University of Utah), umeonesha kwamba watu
wanaopenda kula nyama zilizoiva sana, wako hatarini zaidi kupatwa na saratani
ya njia ya haja kubwa (Rectal Cancer). Hivyo inashauriwa unapopika nyama,
usipike kwenye moto mkali na kuiva kupita kiasi.
POMBE
Unywaji wa pombe kupita kiasi nao unaelezwa
kusababisha aina nyingi ya saratani, kwa wake kwa waume. Aina ya saratani
zinazodaiwa kusababishwa na pombe ni pamoja na satarani ya mdomo, ini, utumbo
na koromeo, ambazo ndizo zinazoua watu wengi hivi sasa nchini Marekani.
NYAMA NA MAFUTA
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Havard
nchini Marekani, umegundua kwamba watu wanaopenda kula nyama kila siku wako
hatarini kupatwa na saratani ya utumbo kuliko wale wanaokula mara moja moja.
Pia baadhi ya mafuta ya wanyama na yale yanayowekwa kwenye ‘baga’ au ‘cheese’
huweza kusababisha kansa.
Vile vile ulaji wa vyakula vilivyotengenezwa
kwa kuchanganya na nyama zilizosindikwa au kuhifadhiwa kwa matumizi ya muda
mrefu husababisha saratani pia. Vyakula hivyo ni pamoja na ‘soseji’ ambazo
hupendwa na watu wengi. Pia mikate ya nyama ‘hot dogs’ nayo ni chanzo cha
magonjwa ya saratani.
VYAKULA VYA UNGA MWEUPE
Vyakula vyote
vinavyopikwa kutokana na unga uliokobolewa na kuondolewa virutubisho vyake
vyote na kuwa mweupe, vinaelezwa kuchangia magonjwa ya saratani kwa kiasi
kikubwa. Vyakula hivyo ni pamoja na ‘donati’ (doughnuts), maandazi, mkate
mweupe, n.k
Mwisho, licha ya kuepuka ulaji wa vyakula
vilivyotajwa hapo juu, unatakiwa kuzingatia ulaji wa vyakula asilia vitokanavyo
na mimea, mboga za majani na matunda kwa wingi kila siku. Utaona kwamba adui
mkubwa wa afya zetu ni vyakula vyote vya kusindika na vile vya kutengenezwa
viwandani au vile ambavyo wakati wa utayarisjaji wake huondolewa virutubisho
vyake vya asili.
0 Comment to "VYAKULA VINAVYOWEZA KUSABABISHA SARATANI"
Post a Comment