Nigeria mabingwa wapya Afrika 2013,yailaza Burkina Faso 1-0
katika mchezo wa fainali nchini Afrika Kusini.
Ni shangwe na vigelegele katika miji mbalimbali nchini Nigeria baada ya timu
yao ya The Super Eagles, kuibuka mabingwa wapya wa Kombe la Mataifa ya
Afrika.
Mbio za kuwania Kombe la Mataifa ya Afrika zilizoanza tarehe 19 Januari
zimehitimishwa, Jumapili, tarehe 10 Februari kwa Nigeria kuibuka bingwa wa
fainali za mwaka 2013 barani Afrika.
Bao la mchezaji Sunday Mba alilofunga katika dakika ya 40 ya kipindi cha
kwanza cha mchezo mjini Johannesburg, ndilo lililowahakikishia The Super Eagles,
Nigeria kuwa mabingwa wapya.
Mchezo huo ulianza kwa kasi, timu zote mbili zikishambuliana kwa zamu. Hata
hivyo Nigeria ndiyo walionekana kutawala zaidi mpambano huo na kukosa magoli
kadha ambayo yangeipa ushindi mnono Nigeria.
Vijana hao wa Super Eagles, wamekuwa wakiimarika kila hatua ya mashindano
hayo, hasa baada ya kufuzu kutoka katika makundi. Ni katika hatua ya makundi
ambapo mabingwa watetezi, Zambia walitolewa na kuachia kombe hilo kufukuziwa na
timu nane zilizoingia robo fainali, na hatimaye timu mbili zilizotinga fainali,
Nigeria na Burkina Faso.
Emmanuel Emenike aliibuka mfungaji bora wa mashindano hayo na kupata kikombe,
huku Moses Victor akiwa mchezaji bora wa mechi kati ya Nigeria na Burkina
Faso.
Mechi hiyo ya fainali ilihudhuriwa na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini, akiwa
mgeni rasmi, akiambatana na rais wa Fifa Sepp Blatter na rais wa CAF, Issa
Hayatou.
The Super Eagles pia waliahidiwa zawadi kem kem, zikiwemo fedha taslim kwa
kocha na wachezaji, hata kabla ya kutwaa ubingwa.
Hii ni zawadi kubwa kwa kocha wa Super Eagles, Stephen Keshi ambaye mwaka
1994, wakati Nigeria ilipotwaa ubingwa wa Afrika, alikuwa nahodha wa timu hiyo
katika fainali zilifanyika nchini Tunisia.
Pia Nigeria ilitwaa ubingwa mwaka 1980, wakati fainali hizo zilipoandaliwa
nchini Nigeria.
Super Eagles kama ilivyo kwa timu nyingine barani Afrika, itakuwa ikijiandaa
kikamilifu kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia zitakazofanyika nchini
Brazil mwaka 2014.
0 Comment to "NIGERIA MABINGWA WAPYA AFRIKA 2013"
Post a Comment